Thursday, January 24, 2013

HOFU YAZIDI KUTAWALA ST JOHN'S , UPORWAJI WAENDELEA

Na Danson Kaijage, Dodoma
HOFU imeendelea kutawala kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha ST John’s   kilichopo mjini Dodoma kutokana na vitendo vya ubakaji na uporwaji mali zao kuendelea.
Hali hiyo ilijitokeza jana baada wanafunzi wa kike katika chuo hicho kuingiliwa katika mabweni yao na mmojawao kubakwa pamoja na kuibiwa laptop tatu,simu tano, fedha taslimu zaidi ya laki moja na elfu ishirini, kamera moja.
Matukio hayo yaliwasababishia wanafunzi hao kufanya maandamano ya amani kwa kulishutumu jeshi la polisi pamoja na uongozi wa mkoa kwa kushindwa kuimarisha ulinzi chuoni hapo.

Wanafunzi wakiwa na mabango yenye maneno mbalimbali  yaliyokuwa  yakisomeka kuwa”Mwogopeni Mungu, polisi mmeshindwa tutajilinda wenyewe,tumekuja Dodoma kusoma siyo kufa , polisi tunakata uwajibikaji au mnawaogopa na maneno mengine ambayo yaliashiria kuwa jeshi hilo limeshindwa kufanya kazi yao kwa uhakika.
Kwa upande wake Makamu wa  Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Liliani Benito akizungumza na wana habari alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kutokuwepo kwa ulinzi makini kati ya jeshi la polisi.
“Hapa yanatokea matukio mengi lakini cha kushangaza wapo watu ambao wanaonekana kufanya vitendo vya wizi hapa chuoni na wanapopelekwa polisi baada ya siku chache unawakuta mitaani na wanaanza kuwatishia wanafunzi kwa majigambo kuwa wao wana mahusiano mazuri na jeshi la polisi hivyo hawawezi kufanywa jambo lolote na jeshi hilo” alisema Lilian.
Alisema kutokana na jeshi la poisi kushindwa kutoa ulinzi wa uhakika chuoni hapo kwa sasa wanafunzi wanahofu ya kuendelea na masomo yao kwani hawana uhakika na maisha yao pindi wawapo chuoni kutokana na vitendo vya ubakaji na wizi ambavyo vinaendelea chuoni hapo.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa chuo hicho, Karimu Meshack, alisema kuwa tukio la mmoja wa wanafunzi kubakwa na wengine kuibiwa lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya watu wasiojulikana kukata nondo ya dilisha walipokuwa wamelala wanafunzi hao na kumuingilia kimwili mmoja wa wanafunzi na wengine kuibiwa.

Karimu akizungumza na waandishi wa habari alisema matukio hayo yanajitokeza kutokana na jeshi la polisi kushindwa kujenga kituo cha polisi chuoni hapo ili kuimalisha ulinzi kwa wanafunzi.

Hata hivyo matukio hayo yalionesha kuwepo kwa mpasuko kati ya uongozi wa chuo na uongozi wa ngazi ya wilaya na Mkoa  kwa kutokuwa na ushirikiano wa kutosha juu ya kupambana na uharifu unaojitokeza chuoni hapo.

Saturday, January 12, 2013

SINGIDA KUANDAMANA KUPINGA KUNYANG'ANYWA ARDHI YAO

WANANCHI  wa maeneo ya Majengo na Kipondoda wilayani Manyoni Mkoani Singida wanatarajia kufanya maandamano makubwa hivi karibuni kupinga hatua ya uongozi wa wilaya kuwanyang’anya maeneo yao na kuyauza kwa watu wengine huku wenye maeneo wakiachwa bila kupewa fidia yeyote.
Mwenyekiti  anayeratibu maandamano hayo, Ufinyu Cheliga akizungumza na Tanzania Daima katka mahojina maalum alisema wanatarajia kufanya maandamano makubwa ya Amani kupinga kunyang’anywa maeneo yao.
Kwa mujibu wa mratibu huyo alisema maeneo hayo wanayamiliki kihalali na wanatarajia kuwakilisha kilio chao hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mratibu huyo pia alieleza kuwa wanakusudia kumwomba mkuu wa mkoa awafukuze kazi Mkurugenzi wa wilaya,Afisa Ardhi  na mwenyekiti wa Halmashauri kwa sababu wao ndiyo chanzo ga migogoro.
 “Hatuna haja tena ya kuendelea kumwambia mkuu wa Wilaya ama mkurugenzi sasa maamuzi yetu ni kuonana na mkuu wa Mkoa na ikishindikana tutaonana na Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi Prof. Anne Tibaijuka na ikishindikana kwake tutapanda hadi kwa Waziri Mkuu na ikishindikana hapo tutamwoma Rais na kama hatutapama majibu tutajua ni jinsi gani ya kuiadhibu serikali…..
“Hatuwezi kuendelea kuteseka wakati ardhi ni yetu na tunayo lakini wapo watu ambao wao ndiyo wanajifanya miungu watu kamwe hatuwezi kukubaliana na jambo hili na ikumbukwe mwaka 2015 siyo mbali kwani mshahara wa dhambi ni mauti” alisema .
Pia alibainisha kuwa wananchi kwa sasa wamekosa imani na mkuu wa wilaya kwani hiyo kutokana na kushindwa kushghulikia migogoro ya ardhi mapema.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa wilaya ya manyoni Fotunata Marya kwa njia ya simu yake ya kiganjani hakuweza kupokea simu kwani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Katika juhudi za kuhakikisha zinapatikana taarifa kutoka kwa walalamikiwa zilifanyika na kumpata Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Manyoni, Leonard Msafiri ambaye alisema kuwa mgogoro hupo lakini unatokana na kuwepo kwa baadhi ya wanasiasa ambao wanachochea tatizo hilo.
Alisema kuwa kutokana na kukua kwa kasi mji wa singida na watu kuendelea na ujenzi holele halmashauri kwa kushirikiana baraza la madiwani waliweka mpango mkakati wa kuanzisha mradi wa upimaji wa viwanja.
“Pamoja na kuwa hatukuwa na fedha lakini kwa kushirikiana na baraza la madiwani pamoja na wananchi ambao wanamiliki mashamba na maeneo makubwa tulikubaliana kupima maeneo ili kuondokana na ujenzi holele…….
“Baadaye tuliomba mkopo wa sh.mil 77 kwa ajili ya upimaji na makubaliano yakawa kila mwenye shamba ama kiwanja kikubwa atapimiwa atapewa viwanja viwili kwanza na vitakavyo baki atauziwa kwa nusu bei tofauti na mtu ambaye ni mgeni na hakuwa na shamba jambo ambalo lilikubaiwa na kamati zote” alieleza msafiri.
Alisema kuwa viwanja vilivyo pimwa ni 740 kutokana na mashamba ya watu na viwanja hivyo vinauzwa kati y ash.laki 270000 na 340,000 na vikubwa vinauzwa katika ya mil.1.6.
Pamoja na wananchi hao kupewa viwajia hivyo lakini wale wote ambao walikuwa na mashamba watalipwa fidia zao kulingana na tathimini iliyofanyika nivyo hakuna mtu ambaye atadhurumiwa.
Naye mkuu wa Wilaya ya Manyoni Fatma Toufiq akiongea katika mahojiano maalum alikiri kuwepo kwa migogoro ya Ardhi na tayari kero zote zimeshafika mezani kwake anazishughulikia na kuhakikisha anazimaliza.

NAIBU WAZIRI KUONGOZA MDAHALO WA REGIA FOUNDATION

NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  katika mdahalo wa Regia Foundation utakaofanyika katika hoteli ya  Peackock iliyopo mnazi mmoja jijini Dar es salaam.
Mdahalo huo unakusudia kuweka kumbukumbu ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Regia Mtema(Chadema) pamoja na kujadili kazi ambazo zilifanywa na mbunge huyo kijana  enzi za uhai wake.
Kwa mujibu wa msemaji wa foundation hiyo Remija Mtema alieleza kuwa founadation  ni asasi iliyoanzishwa kwa lengo la kumuenzi mbunge huyo aliyekuwa kijana na mpiganaji ambapo watafanya mdahalo kwa ajili ya kukumbuka kazi alizozifanya mbunge huyo wakati wa uhai wake.
Remija alidai kuwa wakati wa utumishi wa ubunge wake marehemu Regia aliweza kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto yatima, wahishio katika mazingira magumu pamoja na wale ambao walikuwa wakitokea katika familia masikini.
Kwa mujibu wa msemaji huyo alisema kuwa licha ya Regia kuwa   mbunge wa Viti Maalumu lakini alifanya kazi zake kama vile mbunge wa jimbo kwani alikuwa akijitolea hata katika ujenzi wa shule pamoja na uchimbaji wa visima lakini pia alikuwa anawahudumia watu mbalimbali hususani wenye matatizo sugu ya kiafya.
Remija aliongeza kuwa mdahalo huo pia utajadili nafasi ya utumishi na majukumu ya kijana katika utumishi wake na nafasi mbalimbali za utendaji kazi na umahili wa kijana kufanya kazi.
Aliwataja watakaoendesha mdahalo huo kuwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknologia, January Makamba, mbunge wa Kigoma Kaskazini Zito Kabwe, Mbunge wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila ambaye atasoma historia ya marehemu pia mbunge wa ubungo John Mnyika.
Aidha mada nyingine itakuwa inahusu nafasi ya mtu mwenye ulemavu katika sekta mbalimbali ambapo mada hiyo itatolewa na Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu (CHAWATA) Shida Salum ambayo itakuwa ikilenga kutoa maelekezo na kuonesha wazi kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kufanya kazi za kimaendeleo.
Kwa mujibu wa mtoaji wa taarifa ya foundation alisema kuwa mdahalo huo pia utaanza saa kumi jumatatu na baada ya kumalizika kwa mdahalo kutakuwepo na chakula cha usiku.
Pia alidai kuwa baada ya kumalizika kwa mdahalo huo Jumanne ya  Januari 16, 2013 shughuli zitaamia Kilombero kwa ajili ya upandaji miti katika shule zote za msingi na mgeni rasim atakuwa mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala.