Saturday, January 12, 2013

NAIBU WAZIRI KUONGOZA MDAHALO WA REGIA FOUNDATION

NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  katika mdahalo wa Regia Foundation utakaofanyika katika hoteli ya  Peackock iliyopo mnazi mmoja jijini Dar es salaam.
Mdahalo huo unakusudia kuweka kumbukumbu ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Regia Mtema(Chadema) pamoja na kujadili kazi ambazo zilifanywa na mbunge huyo kijana  enzi za uhai wake.
Kwa mujibu wa msemaji wa foundation hiyo Remija Mtema alieleza kuwa founadation  ni asasi iliyoanzishwa kwa lengo la kumuenzi mbunge huyo aliyekuwa kijana na mpiganaji ambapo watafanya mdahalo kwa ajili ya kukumbuka kazi alizozifanya mbunge huyo wakati wa uhai wake.
Remija alidai kuwa wakati wa utumishi wa ubunge wake marehemu Regia aliweza kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto yatima, wahishio katika mazingira magumu pamoja na wale ambao walikuwa wakitokea katika familia masikini.
Kwa mujibu wa msemaji huyo alisema kuwa licha ya Regia kuwa   mbunge wa Viti Maalumu lakini alifanya kazi zake kama vile mbunge wa jimbo kwani alikuwa akijitolea hata katika ujenzi wa shule pamoja na uchimbaji wa visima lakini pia alikuwa anawahudumia watu mbalimbali hususani wenye matatizo sugu ya kiafya.
Remija aliongeza kuwa mdahalo huo pia utajadili nafasi ya utumishi na majukumu ya kijana katika utumishi wake na nafasi mbalimbali za utendaji kazi na umahili wa kijana kufanya kazi.
Aliwataja watakaoendesha mdahalo huo kuwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknologia, January Makamba, mbunge wa Kigoma Kaskazini Zito Kabwe, Mbunge wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila ambaye atasoma historia ya marehemu pia mbunge wa ubungo John Mnyika.
Aidha mada nyingine itakuwa inahusu nafasi ya mtu mwenye ulemavu katika sekta mbalimbali ambapo mada hiyo itatolewa na Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu (CHAWATA) Shida Salum ambayo itakuwa ikilenga kutoa maelekezo na kuonesha wazi kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kufanya kazi za kimaendeleo.
Kwa mujibu wa mtoaji wa taarifa ya foundation alisema kuwa mdahalo huo pia utaanza saa kumi jumatatu na baada ya kumalizika kwa mdahalo kutakuwepo na chakula cha usiku.
Pia alidai kuwa baada ya kumalizika kwa mdahalo huo Jumanne ya  Januari 16, 2013 shughuli zitaamia Kilombero kwa ajili ya upandaji miti katika shule zote za msingi na mgeni rasim atakuwa mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala.

No comments:

Post a Comment