Thursday, January 24, 2013

HOFU YAZIDI KUTAWALA ST JOHN'S , UPORWAJI WAENDELEA

Na Danson Kaijage, Dodoma
HOFU imeendelea kutawala kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha ST John’s   kilichopo mjini Dodoma kutokana na vitendo vya ubakaji na uporwaji mali zao kuendelea.
Hali hiyo ilijitokeza jana baada wanafunzi wa kike katika chuo hicho kuingiliwa katika mabweni yao na mmojawao kubakwa pamoja na kuibiwa laptop tatu,simu tano, fedha taslimu zaidi ya laki moja na elfu ishirini, kamera moja.
Matukio hayo yaliwasababishia wanafunzi hao kufanya maandamano ya amani kwa kulishutumu jeshi la polisi pamoja na uongozi wa mkoa kwa kushindwa kuimarisha ulinzi chuoni hapo.

Wanafunzi wakiwa na mabango yenye maneno mbalimbali  yaliyokuwa  yakisomeka kuwa”Mwogopeni Mungu, polisi mmeshindwa tutajilinda wenyewe,tumekuja Dodoma kusoma siyo kufa , polisi tunakata uwajibikaji au mnawaogopa na maneno mengine ambayo yaliashiria kuwa jeshi hilo limeshindwa kufanya kazi yao kwa uhakika.
Kwa upande wake Makamu wa  Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Liliani Benito akizungumza na wana habari alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kutokuwepo kwa ulinzi makini kati ya jeshi la polisi.
“Hapa yanatokea matukio mengi lakini cha kushangaza wapo watu ambao wanaonekana kufanya vitendo vya wizi hapa chuoni na wanapopelekwa polisi baada ya siku chache unawakuta mitaani na wanaanza kuwatishia wanafunzi kwa majigambo kuwa wao wana mahusiano mazuri na jeshi la polisi hivyo hawawezi kufanywa jambo lolote na jeshi hilo” alisema Lilian.
Alisema kutokana na jeshi la poisi kushindwa kutoa ulinzi wa uhakika chuoni hapo kwa sasa wanafunzi wanahofu ya kuendelea na masomo yao kwani hawana uhakika na maisha yao pindi wawapo chuoni kutokana na vitendo vya ubakaji na wizi ambavyo vinaendelea chuoni hapo.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa chuo hicho, Karimu Meshack, alisema kuwa tukio la mmoja wa wanafunzi kubakwa na wengine kuibiwa lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya watu wasiojulikana kukata nondo ya dilisha walipokuwa wamelala wanafunzi hao na kumuingilia kimwili mmoja wa wanafunzi na wengine kuibiwa.

Karimu akizungumza na waandishi wa habari alisema matukio hayo yanajitokeza kutokana na jeshi la polisi kushindwa kujenga kituo cha polisi chuoni hapo ili kuimalisha ulinzi kwa wanafunzi.

Hata hivyo matukio hayo yalionesha kuwepo kwa mpasuko kati ya uongozi wa chuo na uongozi wa ngazi ya wilaya na Mkoa  kwa kutokuwa na ushirikiano wa kutosha juu ya kupambana na uharifu unaojitokeza chuoni hapo.


Akizungumza kwa niaba viongozi wa kata ya Kikuyu Kusini Diwani Meja mstaafu Risasi Salingwa, alisema kuwa inasikitisha kuona uongozi wa chuo unashindwa kuwashirikisha viongozi wa kata hiyo na badala yake wamekuwa wakitoa taarifa kwa viongozi wa ngazi ya Wilaya ya Dodoma Mjini,mkuu wa polisi Mkoa na  Mkuu wa Mkoa  na kuwavuka viongozi wa kata jambo ambalo alidai kuwa linaonyesha kuwaepo kwa kuruka ngazi ya kiuongozi.

“Sisi tunawajua wananchi wa kata zetu hapa kikuyu  ni kichaka cha kufuga majambazi na vibaka, ninachoweza kushauri hapa ni kuwa lazima tukae kama kamati uongozi wa chuo na ngazi ya Wilaya na Mkoa ili tuweke mipango mikakati ya kuweza kuongea na wananchi ili kukomesha vitendo hivyo, inabidi mjue kuwa wapo baadhi ya watoto wa viongozi ambao ni waharifu na hivyo wanafichiana siri lakini kama tutashirikiana tutaweza kufichua hali hiyo….

“Mbali  na hilo wanafunzi wenyewe wanapokuwa wamepata fedha zao (Bumu) wamekuwa wakijionesha zaidi na wakati mwingine kuingia katika mambo ya anasa kupita kiasi jambo ambalo jamii inayo wazunguka kujituka wakiingiwa na tamaa na kuanza kuwafanyia vitendo hivyo” alisema.

Kutokana matukio ya mara kwa mara ya wanafunzi kubakwa na kuibiwa mali zao Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk.Rehema Nchimbi ameagiza kituo cha polisi kijengwe haraka chuoni hapo ikiwa ni pamoja na wanafunzi kuzingatia kushiriki vyema katika ulinzi shirikishi.

Kubakwa kwa mmoja wa wanachuo hao pamoja na wengine kuibiwa mali zao kumetokea wakati hivi karibuni mmoja wa wanachuo aliuawa na ambapo mpaka sasa polisi inamshikilia mtu mmoja ambaye anahisiwa kuhusika na mauaji hsayo.

No comments:

Post a Comment