HOFU imeendelea kutawala kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha ST John’s kilichopo mjini Dodoma kutokana na vitendo vya ubakaji na uporwaji mali zao kuendelea.
Hali hiyo ilijitokeza jana baada wanafunzi wa kike katika chuo hicho kuingiliwa katika mabweni yao na mmojawao kubakwa pamoja na kuibiwa laptop tatu,simu tano, fedha taslimu zaidi ya laki moja na elfu ishirini, kamera moja.
Matukio hayo yaliwasababishia wanafunzi hao kufanya maandamano ya amani kwa kulishutumu jeshi la polisi pamoja na uongozi wa mkoa kwa kushindwa kuimarisha ulinzi chuoni hapo.
Wanafunzi wakiwa na mabango yenye maneno mbalimbali yaliyokuwa yakisomeka kuwa”Mwogopeni Mungu, polisi mmeshindwa tutajilinda wenyewe,tumekuja Dodoma kusoma siyo kufa , polisi tunakata uwajibikaji au mnawaogopa na maneno mengine ambayo yaliashiria kuwa jeshi hilo limeshindwa kufanya kazi yao kwa uhakika.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Liliani Benito akizungumza na wana habari alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kutokuwepo kwa ulinzi makini kati ya jeshi la polisi.
“Hapa yanatokea matukio mengi lakini cha kushangaza wapo watu ambao wanaonekana kufanya vitendo vya wizi hapa chuoni na wanapopelekwa polisi baada ya siku chache unawakuta mitaani na wanaanza kuwatishia wanafunzi kwa majigambo kuwa wao wana mahusiano mazuri na jeshi la polisi hivyo hawawezi kufanywa jambo lolote na jeshi hilo” alisema Lilian.
Alisema kutokana na jeshi la poisi kushindwa kutoa ulinzi wa uhakika chuoni hapo kwa sasa wanafunzi wanahofu ya kuendelea na masomo yao kwani hawana uhakika na maisha yao pindi wawapo chuoni kutokana na vitendo vya ubakaji na wizi ambavyo vinaendelea chuoni hapo.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa chuo hicho, Karimu Meshack, alisema kuwa tukio la mmoja wa wanafunzi kubakwa na wengine kuibiwa lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya watu wasiojulikana kukata nondo ya dilisha walipokuwa wamelala wanafunzi hao na kumuingilia kimwili mmoja wa wanafunzi na wengine kuibiwa.
Karimu akizungumza na waandishi wa habari alisema matukio hayo yanajitokeza kutokana na jeshi la polisi kushindwa kujenga kituo cha polisi chuoni hapo ili kuimalisha ulinzi kwa wanafunzi.
Hata hivyo matukio hayo yalionesha kuwepo kwa mpasuko kati ya uongozi wa chuo na uongozi wa ngazi ya wilaya na Mkoa kwa kutokuwa na ushirikiano wa kutosha juu ya kupambana na uharifu unaojitokeza chuoni hapo.