Sunday, November 25, 2012

JESHI LA POLISi LAWAMANI TENA , ASKARI WAKE AUA


JESHI la polisi nchini limeendelea kuandamwa na mzimu wa mauaji ya raia wasiokuwa na hatiai baada askari polisi aliyefahamika kwa jina moja la (Manase) kutuhumiwa kumpiga mwananchi na kusababisha kifo.
Hali hiyo imejitokeza jana katika kituo cha polisi cha Ushirimbo Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, ambapo askari polisi alimpiga risasi na kumuua kijana ambaye alifahamika kwa jina la Rashid Juma (23).
Tukio la polisi kumuua kijana huyo lilisababisha tafrani kubwa baina ya polisi na wananchi wenye hasira kali kwa kuvamia kituo hicho kwa lengo la kulipiza kisasi kwa kuchoma moto kituo hicho na kutaka askari aliyehusika na mauaji ya kijana huyo naye auwawe.
Mbunge wa Bukombe Profesa, Kulikoyela Kahigi(kulia), CHADEMA, akipokea maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe Dk. Archard Rwezahura, aliyevaa shati la kitenge jinsi alivyopokea maiti ya kijana huyo ambaye alipigwa risasi na Polisi na kufikishwa hospitali hapo akiwa amefariki. 
>>>>Hata hivyo askari walilazimika kutumia nguvu nyingi kwa kurusha mabomu ya machozi, risasi za moto na risasi baridi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao ambao walikuwa wakirusha mawe kwa lengo la kuwajeruhi askari hao na  kuharibu mali za kituo hicho.
Tukio hilo lilitokana na askari ambao walikwenda kumkamata mtu ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi na aliyesadikiwa kuwa alikuwa amejificha katika nyumba ambayo ipo katika mtaa wa kilimahewa mjini Ushirombo.
Ambapo askari hao walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumweka ndani ya gari. Baadhi ya wananchi walionekana kulizingira gari hilo huku wakitaka mtuhumiwa huyo atolewe kwenye gari ili auwawe.
Katika kukabiliana na hali hiyo askari walilazimika kufyatua risasi juu kwa lengo la kuwatawanya wananchi na ndipo askari mmoja alipo mlenga kijana huyo risasi ya kiunoni na kijana huyo kupoteza maisha hapo hapo.
Baada ya kuzuka kwa ghasia hizo za wananchi kutaka kuchoma kituo, mbunge wa Bukombe, Peofesa Kulikoyela Kahigi(Cahadema) akiwa ameambatana na Diwani wa kata ya Igulwa, Soud Ntanyagalla (Chadema)walituliza ghasia hizo kwa kuwasii ndugu wa marehemu paomaja na mama yake mzazi Justina Fransis kwa madai kuwa watashughulikia suala hilo.
Mbunge pamoja na Diwani walimtaka mkuu wa Polisi Wilaya kuambatana naye hadi kwenye hospitali ya Wilaya ili kujilidhisha kama kijana huyo ambaye alipigwa risasi kama amefariki ama yuko mahututi.
Viongozi hao walitaka kufika hospitalini hapo kutokana na Mkuu wa Polisi kudai kuwa kijana huyo yupo hai na anaendelea na matibabu.
Hata hivyo baada mbunge na diwani kufika katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe, Mganga Mkuu wa Wilaya Dk.Archard Rwezahura alithibitisha kuwa kijana huyo ambaye alipigwa risasi na polisi alifia mikononi mwa polisi na wala siyo hospitalini kama ilivyokuwa ikidaiwa na jeshi la polisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) Lenard Paul alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kupata taarifa ya kijana huyo kupigwa risasi na kufa,akaahaidi kuwa  hatua za kisheria zitachukuliwa kwa askari aliyehusika.
Kwa upande wa viongozi kwa maana ya Mbunge na Diwani wamewaahidi wananchi kuwa watashughulikia suala hilo na wamelitaka jeshi la polisi lichukue hatua za kisheria kwa askari huyo.

No comments:

Post a Comment